Muimbaji wa muziki wa dansi aliyewahi kutamba akiwa na bendi
mbalimbali zikiwemo Twanga Pepeta na TOT Band, Ramadhan Masanja maarufu
kama Banza Stone amefariki dunia mchana wa Ijumaa, July 17.
Banza alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es
Salaam. Taarifa kuhusu kifo chake zimethibitishwa na kaka yake pamoja
na mmiliki wa Twanga Pepeta, Asha Baraka.
Kwa mujibu wa kaka yake, Jabir
Masanja, msanii huyo alikuwa anasumbuliwa na fangasi kichwani mwake na
dawa alizokuwa anatumia zilikuwa kali kiasi cha kumpotezea hamu ya
kula.
Hivi karibuni mama yake mzazi aliongea na kituo cha redio cha EFM na
kukiambia kuwa afya ya mwanae ilizidi kuzorota na alianza kugoma kula
chakula wala kunywa kunywa dawa. Mama huyo alisema hadi siku hiyo Banza
alikuwa amegoma kula kwa siku tatu mfululizo.
Aliongeza kuwa pamoja na
kuugua hivyo bado wasanii wenzake walishindwa kwenda kumjulia hali.
“Mpaka sasa sijamuona mtu yeyote aliyekuja kumshughulikia na
kumwangalia, wamemwacha hivi hivi. Na mimi siwezi kuwalaumu kwanini
hamjaja kumwangalia, kila mtu na moyo wake, mwenye kuja atakuja, mimi
ntahangaika na mtoto wangu mpaka pale atakapoamua mwenyezi Mungu,”
alisema Mama Banza.
Kabla ya hapo muimbaji huyo alizushiwa kufariki mara nyingi. Wiki
chache zilizopita Banza alimongea na kipindi cha Leo Tena cha Clouds FM
kukanusha.
“Ndio naumwa kichwa kina nisumbua sana lakini sasa hivi naendelea
vizuri yaani hizo habari za kuzushiwa kifo naona sasa hivi kwangu sijui
hata itakuwa mara ya ngapi, maana nimeshazushiwa sana. Mimi mzima na
huyo anayeeneza azunguke na mikoa mingine aeneze vizuri,” alisema Banza.
“Lakini mimi nipo nyumbani hapa Sinza kwa Mama yangu sasa hivi hapa
napata juice yaani marehumu anaongea,” aliongeza Banza kwa kicheko.
“Inshallah nikiwa vizuri mashabiki wangu wataniona tu lakini nipo mzima.”
Msiba upo nyumbani kwao Sinza, Dar es Salaam. Kwa wale wanaopenda
kuchangia msiba wake wanaweza kumchangia kwa kutumia namba: 0715407088
au 0753786016
No comments:
Post a Comment