Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Wednesday, July 22, 2015

Gwajima Asomewa Mashitaka ya Kumtukana Askofu Pengo.......Mashahidi 7 Waandaliwa Kumkabili


Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, jana alikana kutoa lugha ya matusi dhidi ya  Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwamba mtoto, hana akili na mpuuzi.

Askofu Gwajima alikanusha tuhuma hizo wakati akisomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilfred Dyansobera anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo, alidai kuwa kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu katika viwanja vya Tanganyika Packers, vilivyopo Kawe jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alitoa lugha ya matusi kwamba ‘mimi Askofu Gwajima nasema askofu Pengo ni mpuuzi mmoja yule, mjinga mmoja, amekula nini yule, sijui amekula nini yule mtoto hana akili yule’ alinukuu maneno hayo.

Alidai kuwa Askofu Gwajima alitoa maneno hayo yakufadhaisha dhidi ya Askofu Pengo na kwamba yanaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa Machi 27, mwaka huu mshtakiwa alifikishwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa.

Ilidaiwa kuwa alifunguliwa mashitaka na kufikishwa mahakamani dhidi ya tuhuma hizo.

Hata hivyo, Askofu Gwajima alikana mashitaka hayo lakini alikiri majina yake, wadhifa wake, kuhojiwa Kituo cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kweli kanisa lake liko Kawe na kushitakiwa mahakamani hapo.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa unatarajia kuita mashahidi saba na watawasilisha vielelezo vitano.

Wakati huo huo, mahakama hiyo imepiga kalenda kusoma maelezo ya awali ya kesi inayomkabili askofu huyo na wenzake watatu, baada ya mshtakiwa wa nne kuwa mgonjwa.

Kesi hiyo itasikilizwa mbele ya Hakimu Dyansobela Agosti 10, mwaka huu.

Mbali na Gwajima wengine ni  anayedaiwa kuwa mlinzi wake George Mzava,Yekonia Bihagaze  na Georgey Milulu.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa Machi 29, 2015 katika Hospitali ya TMJ iliyopo Mikocheni A, jijini Dar es Salaam,washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakimiliki bastola aina ya Berretta yenye namba ya siri CAT 5802 bila ya kuwa na kibali toka kwa mamlaka inayohusika na silaha  na milipuko.

Alidai kuwa  washtakiwa hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 32 (1) na cha 34 (1)(2) na(3) cha sheria ya Silaha na Milipuko sura ya 223 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.

Upande wa Jamhuri, uliendelea kudai kuwa siku hiyo ya tukio Mzava akiwa na wenzake hao walikutwa wakimiliki isivyo halali risasi tatu za bastola pamoja na risasi 17 za bunduki aina ya Shotgun. Washtakiwa walikana mashitaka yao kwa nyakati tofauti na wako nje kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment