Dar/Arusha. Sasa ni rasmi
kwamba kambi ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Edward
Lowassa imeamua kuachana na chama hicho baada ya madiwani 18 kutangaza
kuhamia Chadema, huku mratibu wa wanachama wanaomuunga mkono kada huyo
wa CCM kuamua kujiunga na vyama vinavyounda Ukawa.
Matukio
hayo yametokea ikiwa ni mwendelezo wa wimbi la wanachama wa CCM
kutangaza kuhamia vyama vya upinzani, hasa Chadema baada ya madiwani
tisa pamoja na wanafunzi 28 wa vyuo vikuu kutangaza kuhamia Chadema
ambayo ni chama kikuu cha upinzani.
Wote wameeleza
sababu ya kuhama CCM ni kutokubaliana na uamuzi wa Kamati Kuu wa kukata
jina la Lowassa wakati wa mchujo wa wagombea urais kwa tiketi ya chama
hicho tawala mwishoni mwa wiki iliyoishia Julai 12.
Akizungumzia
kuhama kwa madiwani hao, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye alisema hawezi kujibu lolote kwa madai kuwa hana taarifa rasmi na
kutaka waulizwe viongozi wa chama wa mkoa.
“Madiwani
hao siwajui na sina taarifa rasmi ninaweza kutoa maoni yangu, lakini
kesho ikabainika kuwa hazikuwa taarifa rasmi juu ya kuhama kwao?”
alihoji.
Nape alisisitiza kuwa hakuna kanuni zilizokiukwa wakati wa kumsaka mgombea urais kama wanachama hao wanavyodai.
Nape
pia alizungumzia kitendo cha mwanasiasa mkongwe, Kingunge
Ngombale-Mwiru cha kuilaumu Kamati ya Maadili na Kamati Kuu akisema
kinaweza kukigawa chama hicho.
“Kama wakiendelea CCM
kitaitisha mkutano na kuwajibu. Lakini kwa sasa tunawataka tu
wawasilishe malalamiko yao sehemu husika maana huo utaratibu wanaujua,”
alisema
Jana, mkoani Arusha, madiwani hao, walioongozwa
na viongozi wa kijadi wa jamii ya Kimasai wanaofahamika kwa jina la
Malaigwanan, walipokewa jana na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Arusha
Mjini, Godbless Lema kwenye hafla fupi iliyofanyika mjini Monduli.
Mwenyekiti wa CCM wa mkoa, Onesmo ole Nangole alisema chama chake hakina uwezo wa kuzuia mtu kuondoka CCM.
“Tumepata
taarifa za kuondoka madiwani na viongozi wetu na kuchomwa kadi lakini
hatuwezi kuzuia uamuzi wa watu kufanya wanachotaka,” alisema.
Alisema
tayari wameanza kufuatilia kinachoendelea kutokea katika maeneo
mbalimbali mkoani Arusha ili kujua athari za matukio hayo kwa CCM.
Viongozi
hao waliohamia Chadema ni 10 wakati Halmashauri ya Wilaya ya Monduli
ina kata 20. Awali, halmashauri hiyo ilikuwa na kata 15 kabla nyingine
tano kuongezwa mwaka huu.
Akisoma tamko la kujiengua
CCM na kuhamia Chadema, mwenyekiti wa madiwani hao, Julius Kalanga
ambaye ni diwani wa Kata ya Lepurko, alisema hatua hiyo imetokana na
kuchoshwa na vitendo alivyoviita vya hila, uonevu, ubaguzi na
unyanyasaji vinavyofanywa ndani ya chama hicho tawala.
“Tumetafakari
usalama wetu ndani ya CCM kwa umoja wetu tumeshindwa kuuona… CCM
iliyokuwa ikiongozwa kwa Katiba, kanuni na miongozo hivi sasa inaongozwa
kwa matakwa ya familia chache kwa jinsi watakavyoona inawapendeza wao,”
alisema Kalanga.
Alisema mchakato wa CCM wa kumpata
mgombea urais uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma ni miongoni mwa
ishara za wazi za chama hicho kukosa maadili kuanzia kwenye vikao vya
Kamati ya Maadili alichodai kilikosa maadili hadi kukatwa kwa majina ya
wagombea akiwemo Lowassa.
Kalanga, mmoja wa wasaidizi
wa karibu wa Lowassa katika shughuli zake za kisiasa, alisema wana-CCM
wamepoteza haki na uwezo wa kuchagua viongozi wanaowataka kutokana na
kunyimwa uwezo wa kufikiri kwa sababu uamuzi hauzingatii utaratibu wa
vikao.
“Tunakataa kuwa watumwa katika misingi hii na
ndiyo maana leo tunaondoka sisi viongozi wote na kuamua kujiunga
Chadema,” alisema Kalanga.
“Tunamwomba Mheshimiwa
Lowassa aungane nasi katika safari yetu hii inayoendelea. Awe na moyo wa
ujasiri na kufanya uamuzi mgumu maana hakuna busara nyingine inayoweza
kutumika zaidi ya kuondoka CCM,” alisisitiza Kalanga.
Diwani
wa Kata ya Mererani, Edward Lenana ambaye ni mmoja wa waliotimkia
Chadema alisema yeye na wenzake watazunguka kwenye majimbo yote ya jamii
ya Wamaasai kuhamasisha jamii hiyo kutochagua wagombea wa CCM kuanzia
ngazi ya udiwani, ubunge na urais.
Akizungumza baada ya
kuwakabidhi viongozi hao kadi za Chadema, Lema aliwataka kuingia kazini
kukijenga chama chao kipya ili kufanikisha ushindi katika uchaguzi mkuu
ujao wa Oktoba 25.
“Ndani ya Chadema hakuna
mheshimiwa, kiongozi wala mwanachama mdogo. Wote ni makamanda wanaopaswa
kupambana dhidi ya uovu na ukandamizaji. Kuanzia leo ninyi nyote ni
makamanda. Hakuna kamanda mgeni wala mwenyeji, bali sote ni wapiganaji
wenye lengo moja la ushindi mwezi Oktoba,” alisema Lema.
Mwenyekiti
wa Chadema wa mkoa, Amani Golugwa aliwataka wanachama hao wapya
kujifunza na kuishi katika misingi ya uadilifu, unyenyekevu na utumishi
kwa umma aliosema ndiyo miongoni mwa imani kuu ya Chadema.
Mbunge
wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na wa viti maalumu, Joyce Mukya
waliwahakikishia viongozi hao fursa ya kuendelea kuwatumikia wananchi
katika kata zao wakiwa Chadema kwa sababu wapigakura ni wale wale, bali
kilichobadilika na jukwaa la kusimamia kuwatumikia.
Wengine Dar wajiengua
Jijini
Dar es Salaam, wanachama waliokuwa kundi la 4U Movement linalomuunga
mkono Lowassa, walitangaza kuihama CCM chama hicho na kujiunga na Ukawa,
kutokana na kile walichodai kuchukizwa na mchakato wa kumpata mgombea
urais.
Mratibu wa wanachama hao, Hemed Ally alisema
wamefikia uamuzi wa kujiunga na Ukawa inayoundwa na vyama vya
NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF, kwa ajili ya “kutafuta mabadiliko nje
ya CCM”, kutokana na kushindwa kuyapata wakiwa ndani ya chama hicho
tawala.
Wadai njama zimewatoa
Wanachama
hao wanaodai wana wafuasi wapatao milioni 10 ambao wengi ni vijana,
walitangaza uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano na
waandishi wa habari, huku wakisisitiza kuwa kulikuwa na njama za
kuhakikisha kuwa Lowassa anaenguliwa huku wakinukuu maneno yaliyosemwa
na kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru ambaye naye
alikilalamikia chama hicho kutomtendea haki Lowassa, ambaye ni mbunge wa
Monduli.
Makada wa CCM waliopitishwa kuwania nafasi ya
kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25
walikuwa 38, huku Dk John Magufuli akiibuka kidedea.
Waliongia tano bora walikuwa Dk Magufuli, Bernard Membe, Balozi Amina Salum Ali, Asha-Rose Migiro na January Makamba.
Wanachama hao walisema kwa pamoja wamekubaliana kutumia kura zao kuking’oa CCM madarakani katika uchaguzi wa mwaka huu.
Ally
alisema kulikuwepo na ukiukwaji mkubwa wa kanuni katika uteuzi, jambo
linalowafanya waamini kuwa Kamati ya Maadili ilikosa maadili.
“Tunaomba
ieleweke wazi hatuna nia ya kumpinga Magufuli ila upatikanaji wake
ulijaa maovu hivyo tumeamua hatutaiunga mkono CCM na kura zetu
tutazipeleka upinzani.
“Lowassa hakutendewa haki na
kila mmoja anatambua hilo, sisi tumeamua kutoka kwa sababu tulikuwa
tunamuunga mkono yeye tukiamini atatuletea mabadiliko lakini kwa mtindo
huu tunaona kiu yetu haiwezi kutimizwa ndani ya CCM,” alisema Ally.
Alivitaka
vyama vya upinzani kuunganisha nguvu kwa pamoja na kushirikiana nao
kuindoa CCM kwa demokrasia ya upigaji kura. Kwa mujibu wa Ally, wafuasi
hao wamegawanyika katika makundi kadhaa ambayo ni 4 U Movement, Lowassa
for Presidency, Team Lowassa, Umoja wa Waendesha Bodaboda na Shirikisho
la Walimu.
“Upinzani ukijipanga vizuri tunaweza kuindoa
CCM madarakani ikizingatiwa kura zetu zote tutazielekeza upande huo
kumuunga mkono mgombea yoyote watakayemsimamisha,” alisema.
Katibu
wa Shirikisho la Walimu Wafuasi wa Lowassa, Maulid Nkungu alisema kama
vijana hawana sababu ya kukubaliana na utaratibu ambao hata wakongwe wa
chama hicho hawajaridhishwa nao.
“Tuliipenda sana CCM,
lakini imeonyesha kutopenda mabadiliko hilo ndilo linalotuondoa
tumechoka kuonewa tunataka kulinda heshima na kuwakomboa
wanaonyanyaswa,” alisema.
No comments:
Post a Comment