MEYA JERRY SILAA AKIWA NA ''TIMU'' YA OFISI YAKE ALIYONENA KWA KINYWA
CHAKE KWA KUKIRI KUSEMA MAENDELEO YA MANISPAA YA ILALA YAMECHANGIWA
SANA NAO KWA KUANZIA DEREVA WAKE ALIYEKUWA ANAMFIKISHA KATIKA MIHADI NA
VIKAO KWA WAKATI NDUGU KASSIM MOTTO, ,MAMA K,JOSEPHINE,JAMAL NA ANTONY
WILLIAM.HII NI PICHA YA KUMBUKUMBU JANA BAADA YA MEYA HUYO KUVUNJA RASMI
BARAZA HILO LA MADIWANI WA MANISPAA YA ILALA AMBAPO PIA AMEWAOMBA
KUMUUNGA MKONO KATIKA HATUA YAKE MPYA YA KUGOMBEA UBUNGE KATIKA JIMBO LA
UKONGA AMBAPO AMEWAAHIDI KUWALETEA MAENDELEO ZAIDI ENDAPO ATACHAGULIWA
KUWA MBUNGE WA UKONGA
MEYA JERRY SILAA AKIFURAHIA BAADA YA KUPEWA BENDERA ALIYOKUWA ANITUMIA
OFISINI KWAKE KWA MIAKA MITANO IKIWA NI ISHARA YA HESHIMA KUBWA KWA
UTUMISHI ULIOTUKUKA KWA WANANCHI WA KATAYA GONGO LAMBOTO NA MANISPAA YA
IALA KWA UJUMLA..MASAMA BLOG INAMTAKIA KIL LA KHERI MEYA JERRY SILAA
KATIKA NDOTO YAKE MPYA YA KUOMBA RIDHAA YA WANCHI KULIWAKILISHA JIMBO LA
UKONGWA KWANI UWEO WAKE HAUNA SHAKA HATA KIDOGO NA TUNAAMINI ATAKUWA
MSAADA MKUBWA KWA TAIFA.
HOTUBA YA MSTAHIKI MEYA MHE. JERRY
SLAA WAKATI WA KUVUNJA BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA
TAREHE 06/07/2015
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilianzishwa rasmi
Mwezi wa Februari 2000, hivyo kufikia mwaka 2015 sasa imetimiza miaka kumi na
tano (15). Katika kipindi chote hicho
zimekuwepo awamu tatu za Uongozi wa
Waheshimiwa Madiwani, ambao ni kuanzia mwaka 2000-2005, 2005-2010 na 2010-2015. Nachukua fursa hii kuwapongeza
Madiwani na Watendeaji wote ambao kwa pamoja walikaa na kuweka mipango
mbalimbali ya kimaendeleo ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Baraza la Madiwani linalomaliza muda wake wa Uongozi
leo tarehe 6/07/2015 ni awamu ya tatu ya Uongozi ulioanza kazi mwaka 2010.
Naamini kuwa kila mmoja atakubaliana na mimi kuwa yapo mafanikio makubwa
yaliyopatikana katika kipindi hiki cha miaka mitano (5). Kupitia miongozo iliyopo ya kuandalia Mipango
na Bajeti ikiwemo-Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010, MKUKUTA, MKURABITA,
Malengo ya malenia na Maelekezo ya Viongozi wa Kitaifa na Baraza la Madiwani,
Halmashauri imetekeleza vyema azma ya kupeleka maendeleo kwa wananchi wake na
kwa mujibu wa Dira ya Halmashauri isemayo;
“Kuwa na Jamii yenye maisha bora
ifikapo mwaka 2025”.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Manispaa
ya Ilala kupitia Idara mbalimbali na Vitengo vyake imeweza kutekeleza Dira yake
kwa ufanisi. Mafanikio haya yanaonekana katika maeneo yafuatayo;
UKUSANYAJI WA MAPATO
Ili
kuweza kutekeleza majukumu yake, Halmashauri inapaswa
kuhahikikisha inakusanya mapato ya kutosha, hususani ya ndani
kuwezesha
utoaji wa huduma kwa wananchi wake kupitia utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
Kwa kila mwaka katika kipindi cha
miaka mitano (5) Halmashauri ya Manispaa imekuwa ikiongeza juhudi za
kukusanya mapato yake ya ndani. Katika
mwaka wa fedha wa 2010/2011 Halmashauri ilikisia kukusanya jumla ya
Sh. 16,110,130,000,
mapato halisi yaliyokusanywa mwisho wa mwaka yalifikia Sh.
13,059,508,452 sawa na Asilimia 81% ya lengo lake. Kiwango hicho
kimekuwa kinaongezeka na kufikia mwaka huu wa fedha
2014/2015, makisio yalikuwa ni Sh. 30,450,000,000 hadi kufikia Juni,
2015 makusanyo
halisi yamefikia Sh. 30,862,178,729.90 sawa na Asilimia 103 ya lengo
la mwaka.
Aidha kwa mwaka unaofuata wa 2015/2016 Halmashauri imepanga kukusanya
Sh. 54,258,100,000
kutoka mapato ya ndani. Jambo kubwa linalochangia mafanikio haya ni
kuboreshwa kwa zoezi la kukusanya Takwimu za walipa kodi, mpango
unaolenga kubaini idadi ya walipa
kodi wa Halmashauri na hivyo kuwa na makadirio halisi ya mapato. Aidha
kutokana
na kukua kwa Tekinolojia ya mawasiliano Manispaa imeanza kuwasiliana
na
Walipa kodi wake kwa njia ya simu zao za mkononi kwa ajili ya
kuwahimiza na
kuwakumbusha ulipaji wa Kodi/Tozo na Ushuru mbalimbali.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Usimamizi mzuri ambao umekuwa ukifanywa na Waheshimiwa Madiwani katika
kuhakikisha kuwa kanuni za matumizi ya fedha zinazingatiwa, umeiwezesha Halmashauri kuendelea kupata Hati safi za
Ukaguzi wa Mahesabu. Uthibitisho wa karibu ni taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali ya mwaka wa fedha wa 2014/15 ambapo Manispaa ya Ilala ni miongoni
mwa Halmashauri zilizopata hati safi ya Mahesabu.
MASOKO
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
|
Manispaa
ya Ilala ina jumla ya masoko 18, masoko makubwa ni Matano (5), masoko
madogomadogo ni 8 na maeneo matano (5) yasiyotumika kikamilifu. Kati ya masoko
matano makubwa, masoko matatu (3) ya Kisutu, Ilala na Buguruni ni masoko
yaliyojengwa miaka ya 1960 hivyo kwa sasa hayakidhi mahitaji makubwa ya
Wafanyabishara walioko katika masoko hayo. Katika kipindi hiki cha miaka mitano
Halmashauri ya Manispaa imeweka mazingira mazuri kwa ajili ya maendeleo
endelevu ya Sekta za
Biashara na Masoko kwa lengo la kuzalisha ajira, hususani kwa wafanyabiashara
wadogo. Halmashauri imeweza kuanisha
maeneo 17 ya kuendelezwa ikijumuisha shughuli za wafanyabiashara wadogo. Lengo kuu likiwa kuwafanya wafanyabiashara
wadogo kuondokana na uchuuzi mdogo mdogo
na kuwa wajasiriamali. Aidha Halmashauri imesaini Mkataba na Benki ya
Rasilimali (Tanzania Investment Bank-TIB) kujenga soko la kisasa la Kisutu, baadaye
masoko ya Buguruni na Ilala yataendelezwa.
ELIMU YA MSINGI NA SEKONDARI
|
|
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Manispaa ya Ilala imefanikiwa katika utoaji wa Elimu ya Msingi na
Elimu ya Sekondari kwa wananchi wake. Katika kipindi hiki cha miaka mitano
jitihada mbalimbali zimefanyika za kukabiliana na changamoto zinazoikabili
Sekta ya Elimu. Pamoja na juhudi za
Serikali Kuu na Halmashauri, wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kuboresha
Sekta hii. Mashirika ya simu ya Vodacom Foundation, Tigo, Benki Kuu na KCB ni miongoni mwa waliochangia
samani katika shule mbalimbali za Msingi. Aidha Ofisi yangu kupitia ”Mayors Ball” na Mpango uliobuniwa na Mhe Diwani wa
Kipawa umezipatia baadhi ya shule madawati. Mpango wa Mnazi Mkinda wa kuibua
vipaji mbalimbali kwa wanafunzi wa shule ya Msingi nao umechangia kuboresha sekta
hii. Kwa takwimu zilizopo katika kipindi husika madawati 32,021 yamenunuliwa katika jitihada za kukabiliana na upungufu wa
madawati. Vyumba vya madarasa 111 na Matundu ya vyoo 2109 yamejengwa
katika shule za msingi. Watoto 4,876
wa elimu ya awali na 21,798 wa elimu
ya msingi waliandikishwa kuanza masomo mwaka 2015, Hali hiyo imechangia ufaulu wa shule ya
msingi kupanda kutoka chini ya Asilimia 58 mwaka 2010 kufikia Asilimia 70.5 mwaka
2014. Aidha ujenzi wa vyumba 76 vya madarasa na maabara 154 katika shule za
Sekondari umekamilika kwa asilimia 98. Nachukua nafasi hii kuwapongeza
Madiwani wajumbe wa Kamati iliyosimamia masuala ya Elimu, Mkurugenzi wa
Manispaa na Wataalam wake kwa kuhakikisha mipango ya elimu inatekelezwa kwa
ufanisi.
HUDUMA ZA AFYA
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika eneo la Afya yapo mafanikio makubwa
yaliyofikiwa. Kwa mujibu wa Takwimu zilizokuwepo mwaka 2010 kulikuwa na jumla ya zahanati, vituo vya
Afya na Hospital 19 ambapo hadi
kufikia mwaka 2015 vimeongezeka na kufikia
29. Aidha katika kipindi hiki baadhi ya Hospitali na Zahanati zimeingizwa
kwenye mchakato wa kupandishwa hadhi. Hospitali ya Amana imepanda hadhi na sasa ni
Hospital ya Mkoa ambapo Kituo cha Afya Mnazi Mmoja kimepandishwa hadhi kuwa
Hospital. Zahanati ya Pugu Kajiungeni
inaendelea na mchakato wa kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya. Kumekuwa na
kuimarika kwa ushirikiano kati ya Idara ya Afya na Wadau wa Afya hususan Taasisi
zinazojihusika na utoaji wa Tiba. Utoaji wa Chanjo kwa Watoto na Kina Mama
Wajawazito umevuka lengo la Kitaifa la asilimia 90 na kufikia asilimia 100
kwa chanjo karibu zote. Mafanikio haya yote yanaonesha ni jinsi gani
Waheshimiwa Madiwani pamoja na Watendaji wameweza kuelekeza jitihada zao katika
eneo hili muhimu la huduma linalogusa moja kwa moja maisha ya Wananchi, kwani
inaaminika kuwa Mtu mwenye Afya bora anao mchango mkubwa katika familia yake
na Taifa lake.
USAFI NA HIFADHI YA MAZINGIRA
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika eneo hili, Halmashauri inaendelea na juhudi za kuliweka Jiji katika hali ya
usafi. Takwimu zinaonesha wakazi
wa Manispaa ya Ilala wanazalisha tani 1,100 za taka ngumu kila siku wakati
uwezo wa kuzoa na kusafirisha hadi dampo la Kigogo Fresh katika Kata ya Pugu ni
Tani 676 kufikia Juni, 2015 kiwango
hicho ni sawa na Asilimia 61% ya uzalishaji. Mwaka 2010 Halmashauri pamoja na
Wakandarasi wengine wa kuzoa taka waliweza kuzoa wastani wa Asilimia 50% za
taka ngumu kwa siku. Aidha Halmashauri
ina uwezo wa kufagia Km. 136 za barabara kwa siku dhidi ya Km. 126 za mwaka
2010. Uwezo huu mdogo wa uzoaji wa
taka umechangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa vitendea kazi hususani,
malori yenye uwezo mkubwa wa kuzoa taka. Baraza hili la Madiwani linavunjwa likiwa
tayari limetoa idhini ya kukopa Sh. 2.55 Bilioni kwa ajili ya kununua malori
17 ya kusafirisha taka ili kuboresha zaidi hali ya usafi Jijini.
Kwa kushirikiana na Sekta binafsi Halmashauri
inaendelea kutunza jumla ya Ha. 137.4 za misitu katika bonde la Zingiziwa,
Kinyerezi, Kivule dhidi ya majanga ya moto na uvunaji usio endelevu wa mazao
ya misitu. Vikundi 7 vinaendelea na ufugaji nyuki kutumia mizinga ya 157
iliyotundikwa katika misitu ya asili, na ya kupandwa katika maeneo mbalimbali
ya Manispaa. Kupitia Kamati za
mazingira za Kata, Wananchi wamekuwa wakielimishwa juu ya umuhimu wa kutunza Vyanzo
vya maji na Uoto wa asili hususani kwenye maeneo ya miinuko.
MIPANGOMIJI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Kama inavyofahamika Manispaa ya Ilala ndiyo yenye kubeba taswira ya Jiji
la Dar es Salaam, hivyo katika kipindi hiki cha miaka mitano (5) jitihada zimefanyika za kuhakikisha kuwa
ujenzi wa nyumba na majengo unazingatia Sheria na kupunguza makazi holela.
Kumekuwa na mipango ya kubadilisha taswira ya eneo la Manispaa ambapo mipango
ya uendelezaji upya wa maeneo mbalimbali imeidhinishwa. Jumla ya viwanja 29,243 vimemilikishwa kwa wananchi na viwanja 9,123 vimepimwa katika maeneo ya umma, leseni mpya za makazi 1,568 zimesajiliwa.
Aidha wananchi 62,000 wamepata elimu ya sheria za ardhi, Mipango miji na
matumizi bora ya ardhi.
UJENZI WA MIUNDOMBINU
Kupitia Idara ya Ujenzi, Halmashauri ya Manispaa imeweza kuboresha
zaidi miundombinu yake ya Barabara, ambapo imeweza kuongeza urefu wa Km. 71.31 za barabara za lami kutoka
jumla ya Km. 190.32 zilizokuwepo mwaka 2010 kufikia Km. 261.63 mwaka
2015. Urefu wa barabara za Changarawe
umeongezeka kwa Km. 56.77 kutoka Km. 76.6 za mwaka 2010 kufikia Km. 133.37
mwaka 2015 na barabara za udongo zenye urefu wa Km. 638.95. zimetengenezwa. Aidha, makalavati 37 nayo yameweza kujengwa. Katika kipindi hiki Manispaa imeweza kununua
Greda mbili (2) kwa njia ya mkopo ikilenga kuhakikisha kuwa barabara zake
zote zinapitika katika vipindi vyote vya mwaka.
HUDUMA ZA MAJI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Sote tunatambua kuwa maji ni rasilimali muhimu. Katika kipindi hiki cha miaka mitano (5) jitihada
za kusambaza maji safi na salama katika Manispaa zimefanyika ambapo Halmashauri
imechimba visima virefu 42 na kufanya jumla ya visima vyote vilivyopo kufikia 247. Visima vifupi nane (8) vilichimbwa na kufikia jumla ya
visima 69. Vituo vya kuchotea maji
1,239 Mifumo 9 ya kuvuna maji ya mvua imejengwa. Vikundi vya watumia maji 15 na kamati za
maji 50 zimeundwa. Hadi kufikia Juni, 2015
idadi ya wakazi wanaopata maji safi na salama wanaohudumiwa na visima vya
Halmashauri wamefikia Asilimia 52% ya wakazi wote wa Manispaa wanaokadiriwa
kuwa 1,220,611 (Sensa ya 2012).
MAENDELEO NA USTAWI WA JAMI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika kipindi cha kuanzia 2010 hadi 2015 Manispaa ya Ilala
imeendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya Ustawi wa Jamii ambapo upo mfumo
mzuri wa kuendeleza vikundi vya Wanawake na Vijana. Makundi haya yamekuwa
yakinufaika kwa kupatiwa mikopo kutoka Benki yetu ya DCB ambapo Halmashauri
ina hisa, pia Mfuko wa Wanawake na Vijana umeendelezwa kwa Halmashauri
kutenga fedha kukopesha makundi hayo. Hadi kufikia Juni 2015 vikundi 37 vilifikia hatua za mwisho za kukopeshwa mitaji ya
biashara. Aidha Manispaa ya Ilala imeweka mfumo mzuri wa kuhudumia Watoto
waishio katika mazingira hatarishi kupitia Timu ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto.
Dawati la kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu
lililofunguliwa Hospital ya Amana limewezesha kuokoa idadi kubwa ya Watoto
waliokuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia.
MAHUSIANO NA WADAU
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Tunapopima
mafanikio ya Manispaa ya Ilala hatuwezi kuacha kuzungumzia eneo la
mahusiano. Dhana ya maendeleo kwa njia
ya kushirikisha Wadau wakijumuisha Wafadhili imeendelea kutekelezwa ndani ya
Manispaa ya Ilala. Ofisi ya Mstahiki Meya
imeweza kushawishi Shirika la KOICA kujenga Hospitali eneo la Chanika.
Mkataba wa Makubaliano ya kuanza ujenzi umeshasainiwa. Ujenzi wa Hospital hii
utasaidia kusogeza huduma karibu na Wananchi na kupunguza msongamano wa
Wagonjwa katika Hospitali ya Amana. Katika kipindi hiki mipango ya Maendeleo
inayoibuliwa imekuwa Shirikishi. Kata zote 26 zimeunda Kamati ya wananchi
zenye jukumu kuu la kuibua vipaumbele vya ngazi ngazi ya Kata ambavyo baada
ya kuidhinishwa na Kamati za Maendeleo za Kata inajumuishwa katika Mipango na
Bajeti ya Halmashauri ambako inatengewa fedha. Aidha Halmashauri imesimamia na kuendeleza
mahusiano yaliyopo kati ya Manispaa ya Ilala na Mji wa Kokkola ulioko
Finland.
KUTANGAZA SHUGHULI MBALIMBALI ZA
HALMASHAURI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeweza kuweka mahusiano mazuri na
vyombo vya Habari ambavyo vimekuwa vikiuhabarisha umma masuala mbalimbali
yanayotokea na yanayoihusu Manispaa ya Ilala.
Katika kujitangaza huko Halmashauri inalo Jarida lake ambalo limekuwa
likitangaza kazi mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa. Aidha kupitia mitandao ya kijamii Manispaa
imeanzisha Blog - Habari ilala.Blogspot.Com ambayo hadi kufikia Juni 2015
jumla ya wanaoingia katika mtandao huo imefikia 30,000 kutoka pande zote za
dunia.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Napenda kumalizia hotuba yangu kwa kusema kwamba, Baraza hili la
Madiwani la Awamu ya tatu ya Uhai wa Halmashauri linavunjwa likiwa lina mambo ya kujivunia
hususani katika kuandaa mazingira endelevu ya Uwekezaji, Kuongezeka kwa
mapato ya ndani, Uboreshaji wa huduma za Kiuchumi, elimu na Afya. Nampongeza
Mkurugenzi na timu yake ya wataalam, Waheshimiwa Madiwani wote, Uongozi wa
Wilaya, Uongozi wa Mkoa na wataalam wake. Ushirikiano wa karibu wa timu hii
umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio tunayoyaona kwa sasa. Naamini Awamu ya
nne ya Uongozi unaokuja utaanzia mahali pazuri.
Ahsante sana kwa kunisikiliza.
Jerry Silaa
MEYA WA MANISPAA
HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA
|
No comments:
Post a Comment