Watu 150 wameuawa baada ya Boko Haram kuvamia kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Walioshuhudia
mashambulizi hayo wanasema watu tisini na saba wameuawa siku ya
Jumatano katika kijiji cha Kukawa kilichopo karibu na Ziwa Chad.Habari zinasema pia wanaume 48 wamepigwa risasi na wapiganaji katika mashambulizi tofauti siku ya Jumanne.
Mashuhuda wanaokimbia eneo lililopo karibu na Ziwa Chad wanasema idadi kubwa ya wapiganaji wamevamia vijiji vitatu ambapo wameuwa wanaume, wanawake na watoto.
Baadhi ya ripoti zinasema walipigwa risasi huku wengine wakielezea jinsi wapiganaji hao walivyowachinja watu na kuchoma majengo.
Upande wa Kusini, nje kidogo na mji wa Monguno, kundi la wapiganaji wa Boko Haram wamefika usiku wakati watu walipokuwa wanaswali. Waliwasubiri mpaka walipomaliza kuswali na kuwatenganisha wanaume na wanawake na baadae kuanza kuwamiminia risasi wanaume.
Mwanasiasa anayewakilisha eneo hilo, Mohammed Tahir amesema awali alitoa tahadhari kwa jeshi la Nigeria kwamba vijiji hivyo viko hatarini kwa sababu Boko Haram wameweka makazi katika maeneo hayo baada ya kutimuliwa katika himaya yao ya msitu wa Sambisa.
Haya ni mashambulizi mabaya zaidi kufanywa na Boko Haram katika kipindi cha wiki kadhaa.
Kundi hilo limekuwa likilipuwa mabomu kadhaa baada ya kudhoofishwa na majeshi ya Nigeria.
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari amesema kipaumbele chake ni kuimarisha mapambano dhidi ya Boko Haram.
No comments:
Post a Comment