BAADA ya vuta nikuvute
katika vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
kuhusu kukubaliwa au kutokubaliwa kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Ngoyai
Lowassa kujiunga na umoja huo ili kuongeza nguvu ya kisiasa, hatimaye
mwanasiasa huyo maarufu nchini amekubaliwa na tayari amejiunga rasmi
Ukawa akiwa mwanachama halisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), imefahamika.
Taarifa rasmi kutoka Ukawa na kwa msemaji wa Lowassa ambaye hakutaka
jina lake litajwe, imeeleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa baada ya
majadiliano ya kina katika Mkutano Mkuu wa Ukawa uliofanyika mapema wiki
hii huku ajenda kubwa ikiwa ni kumpokea Lowassa ili kuimarisha kambi ya
upinzani ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kama mgombea urais wa umoja
huo.
Taarifa rasmi zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa Lowassa
anatarajiwa kutangazwa rasmi Jumapili hii hivyo maadalizi ya mkutano
mkubwa wa aina yake yanaendelea. Chanzo chetu kutoka katika mkutano huo
kilisema kwa moyo mmoja, wenyeviti wa vyama vyote vinavyounda umoja huo,
yaani Freeman Mbowe (Chadema), Profesa
Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCRMageuzi) na Emmanuel Makaidi
(NLD), wameridhia kuungana na Lowassa katika safari yao ya kuking’oa CCM
madarakani huku wakiamini kuwa wakimsimamisha kuwa mgombea wa Ukawa
watafanikisha azma ya vyama vya upinzani kuingia ikulu.
“Katika kikao chetu tulijadili mikakati kadhaa ya kuchukua dola lakini
kubwa zaidi lilikuwa ni jinsi ya kuungana na Lowassa ili kutimiza azma
hiyo, ikizingatiwa kwamba hivi sasa anaungwa mkono na Watanzania wengi
na hasa jinsi ambavyo hawakuridhishwa na mchakato wa kumuengua kuwania
urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo tuna uhakika kwa
mkakati huu lazima tuking’oe CCM madarakani,” alisema mjumbe mmoja wa
Mkutano Mkuu (jina limehifadhiwa).
TUNDU LISSU AFUNGUKA
Akizungumzia suala hilo, Mnadhimu Mkuu wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, aliliambia gazeti hili kuwa
majadiliano kuhusu Lowassa yalikuwa ya lazima kwa kuwa katika muungano
wa vyama kila kiongozi ana mtazamo wake hivyo, kila jambo la muhimu
lazima lifanyike kwa majadiliano ili kufikia mwafaka kwani lengo ni
kuhakikisha kwamba kunakuwapo na mkakati wa pamoja kuhakikisha kuwa CCM
kinag’olewa madarakani ili makada wa chama hicho waelewe kuwa sasa
Watanzania wanahitaji mabadiliko na si maneno matupu ya majukwaani.
LIPUMBA NAYE ANENA
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema kwamba Ukawa hivi sasa wamejipanga kimkakati kuhakikisha
wanachukua dola na kuongeza kwamba waliokuwa wakieneza propaganda kuwa
anawakwamisha wataendelea kuumbuka kwa kuwa vyama vyote vinavyounda
Ukawa ni kitu kimoja.
Aliongeza kwamba, kamwe umoja huo hauwezi kusambaratika kwani ajenda kuu
ni kuindoa CCM madarakani na kuongeza kwamba, mambo mengine kama
mgawanyo wa ruzuku yatafuata baadaye kwani yanazungumzika katika ngazi
ya uongozi.
MSIMAMO WA LOWASSA
Msemaji wa Lowassa ambaye kawa sasa ndiye gumzo la taifa ukiachana na
Dk. John Magufuli aliyepitishwa na CCM kuwania kiti cha urais
amelihakikishia gazeti hili kuwa Lowassa ameamua kuingia Ukawa ili
kuendeleza siasa za kistaarabu kutimiza azma yake ya Safari ya Matumaini
kama ambavyo amekuwa akiwaahidi Watanzania.
Alisema ameamua kuungana na Ukawa kwa kuwa anaamini kuwa lengo la vyama
vyote vya siasa ni kuhakikisha vinatimiza malengo yao ya kuwahudumia
wananchi, hivyo inapotokea katika chama kimojawapo, bado kuna nafasi ya
kutumia vyama vingine kutimiza malengo ya kisiasa. Msemaji huyo
aliongeza kwamba baada ya kuenguliwa alikuwa na kazi ngumu ya kubaini
nini cha kufanya ili kutimiza azma yake ya kisiasa, ndiyo maana alikaa
kimya ili kuepusha mivutano kati yake na CCM lakini hakuwa amekata tama
kuhusu jinsi anavyoweza kuwakomboa Watanzania kutoka katika dimbwi la
umaskini, jambo ambalo alikuwa akiwaeleza katika safari yake ya kusaka
wadhamini nchi nzima.
MKAKATI WA KAMPENI
Msemaji huyo alisema kuwa akiwa katika Ukawa, Lowassa ameandaa mkakati
kabambe wa uhamasishaji wananchi ili watambue kwamba azma ya kuwakomboa
ipo palepale na kuongeza kuwa ana uhakika watamuunga mkono kwani
anatambua kwamba wapo pamoja naye katika safari ya matumaini.
Alisema kwamba kazi iliyo mbele yake ni kuhakikisha kuwa anaisuka upya
‘Team Lowassa’ na atakuwa makini na baadhi ya watu waliomsaliti ili
wasiharibu mkakati wake na kuongeza kwamba watazunguka nchi nzima
kufanya kampeni za kistaarabu, zisizokashfu wanasiasa wengine ili
wananchi wapime ni kiongozi gani anafaa kati ya yeye na wengine.
TATHMINI YA USHINDI
Chanzo chetu ndani ya Ukawa kilieleza kwamba, tathmini iliyofanywa hadi
sasa inawapa uhakika wa kuchukua dola kwani katika maeneo mengi, Lowassa
anaungwa mkono zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote yule. Kilisema kuwa
katikamaeneo mengi CCM haikubaliki kutokana na kuendesha siasa za
kibabe na mizengwe, jambo ambalo limekuwa likiwakera wananchi kwani
kinachotokea ni kwamba wanachaguliwa viongozi badala ya wao kuchagua
viongozi wanaowataka.
Kilisema Lowassa ana nguvu zaidi katika Mikoa ya Kaskazini, Kanda ya
Ziwa, Kusini, Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar hivyo CCM kama inataka
kushindana naye ijipange vyema.
ZITTO AJUMUISHWA
Katika mkakati huo wa ushindi, inaelezwa kwamba, umoja huo utamjumuisha
kundini Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye
chama chake nacho kitaongeza nguvu ya ushindi.
Lowassa alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM kati ya wagombea 38
ambao walichukua fomu lakini jina lake lilikatwa katika kikao cha Kamati
ya Maadili na Usalama ya CCM, jambo ambalo lilizua sintofahamu miongoni
mwa wanasiasa wengi waliokuwa wakimuunga mkono, hatua ambayo
ilisababisha mtikisiko wa kisiasa nchini.
No comments:
Post a Comment