MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imeshindwa kumsomea maelezo ya awali Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya matusi na kushindwa kuhifadhi silaha.
Kesi hiyo ilitajwa jana kwa ajili ya washitakiwa kusomewa maelezo ya
awali lakini iliahirishwa kwa kuwa Hakimu Mkazi Wilfred Dyansobera
anayesikiliza kesi hiyo hakuwepo mahakamani.
Hakimu Mkazi, Thomas Simba aliahirisha kesi hiyo hiyo Julai 20, mwaka
huu kwa ajili ya washitakiwa hao kusomewa maelezo ya awali mbele ya
Hakimu Dyansobera.
Mbali na Gwajima washitakiwa wengine, ni Mlinzi wake, George Mzava,
Msaidizi wake, Yekonia Bihagaze (39) na Mchungaji Georgey Milulu (31)
wanakabiliwa na shitaka la kukutwa na silaha pamoja na risasi kinyume
cha sheria.
Katika kesi ya kwanza namba 85, Gwajima anadaiwa kati ya
Machi16 na 25, mwaka huu katika Viwanja vya Tanganyika Packers Wilaya ya
Kinondoni Dar es Salaam alitoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu wa
Kanisa Katoliki Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akimueleza Askofu
kwamba ni mtoto, mpuuzi asiye na akili katika namna ya kwamba ingeleta
uvunjifu wa amani.
Katika kesi nyingine namba 84 , Gwajima anakabiliwa
na mashitaka ya kushindwa kuhifadhi silaha na risasi jambo ambalo ni
kinyume cha sheria ya uhifadhi wa silaha za moto.
Anadaiwa kati ya Machi
27 na 29, mwaka huu, ndani ya Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, alishindwa
kuhifadhi silaha aina ya Beretta namba CAT 5802, risasi 3 za pisto na
risasi 17 za shotgun.
Katika mashitaka mengine yanayowakabili
washitakiwa wengine, inadaiwa Machi 29, mwaka huu katika Hospitali ya
TMJ Mikocheni ‘A’ walikutwa wakimiliki silaha na risasi hizo bila ruhusa
kutoka mamlaka husika.
No comments:
Post a Comment