Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Tuesday, July 7, 2015

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza Ashitakiwa Mahakamani Jijini Arusha Kwa Kukiuka Katiba Ya Nchi Hiyo


Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza ameshitakiwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki iliyopo jijini Arusha kutokana na hatua yake inayotajwa kukiuka Katiba ya nchi hiyo kwa kuwania kipindi cha tatu cha Urais.
 
Kesi hiyo pia inamjumuisha Mwanasheria Mkuu wa Burundi, Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi kwa nchi ya Burundi pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mujibu wa taarifa maalum kutoka kwenye taasisi ya mawakili wa Kanda ya Afrika (PALU) inayosimamia shauri hilo.
 
Hii sasa inamaanisha kuwa kiongozi huyo wa Burundi atahitajika wakati wowote kwenda Arusha mahakamani, kuhudhuria kesi yake.
 
Ripoti hiyo iliyoidhinishwa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha PALU, Jancelline Amsi, imeeleza kuwa shauri hilo namba RCCB 303 la 2015 dhidi ya Nkurunziza liliwasilishwa katika Mahakama ya Jumuiya na Umoja wa mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi na Tanzania chini ya mwamvuli wa taasisi yao ya ‘East African Civil Society Organizations’ Forum (EACSOF).
 
Mashirika hayo yanamtuhumu Rais Nkurunziza kwa kukiuka katiba ya nchi yake pamoja na kuvunja makubaliano ya Amani ya Arusha katika dhamira yake ya kugombea urais kwa kipindi cha tatu, hatua ambayo imesababisha machafuko nchini Burundi yaliyopelekea vifo vya wananchi wapatao 70 huku wengine zaidi ya 140,000 wakiikimbia nchi yao.
 
Hatua hiyo inakuja wakati Rais Nkurunziza akiwa amejikita katika kampeni za urais, hivyo kushindwa kujumuika na wakuu wa nchi za EAC wanaokutana Dar es Salaam kujaribu kutafuta ufumbuzi wa tatizo la kisiasa la Burundi.
 
Msemaji wa Rais Nkurunziza, Gervais Abahiro alieleza kutoka Bujumbura alisema kuwa bosi wake huyo angewasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Alain Aime Nyamitwe kwani Rais wake alikuwa anaendelea na kampeni zake za urais.

No comments:

Post a Comment