Edward Ngoyayi Lowassa (Chadema) - Rais
Profesa Nguyulu Ibrahim Haruna Lipumba (CUF) - Makamu
Freeman Aikaeli Mbowe (Chadema) - Mambo ya Nje
John John Mnyika (Chadema) - Fedha na Uchumi
David Kafulila (NCCR-Mageuzi) - Kazi na Ajira
David Ernest Silinde (Chadema) - Tamisemi
Dk. Emmanuel John Makaidi (NLD) - Viwanda, Biashara na Masoko
James Mbatia (NCCR-Mageuzi) - Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Joseph Selasini (Chadema) - Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu)
Magdalena Hamisi Sakaya (CUF) - Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
Masoud Abdallah Salim (CUF) - Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano)
Mchungaji Peter Simon Msigwa (Chadema) - Maliasili na Utalii
Mhandisi Mohammed Habib Juma Mnyaa (CUF) - Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu
Pauline Phillipo Gekul (Chadema) - Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji)
Prof. Kulikoyela Kanalwanda Kahigi (Chadema) - Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma)
Rajab Mohammed Mbarouk (CUF) - Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge)
Tundu Antipas Lissu (Chadema) - Sheria na Katiba
Wilfred Muganyizi Lwakatare (Chadema) - Ofisi ya Rais (Utawala Bora)
Na Daniel Mbega
UKAWA
wameokota almasi kwenye mchanga wa pwani, na kwa kumpata Edward Lowassa
Umoja huo wa Katiba ya Wananchi unaamini utachukua dola ifikapo Oktoba
25 mwaka huu.
Lowassa,
waziri mkuu aliyelazimika kujiuzulu kufuatia kashfa ya kinyonyaji ya
kampuni za ufuaji umeme wa dharura za Richmond na Dowans, ameshawishika
kujiunga na umoja huo kupitia Chadema, hali ambayo wachambuzi wengi wa
masuala ya siasa wanasena kuna kila dalili za kuung’oa utawala msonge wa
Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho huenda baada ya Oktoba itabidi kiunde
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB).Duru za siasa kutoka ndani ya
Ukawa zinaeleza kwamba, ilikuwa kazi ngumu kumshawishi Lowassa kuhamia
Ukawa baada ya kuenguliwa na CCM katika kinyang’anyiro cha urais, lakini
kwa sasa kazi itakuwa rahisi zaidi kushinda uchaguzi wa mwaka huu
kutokana na mwanasiasa huyo kuwa na wafuasi wengi nyuma yake.
Mchakato
unaoendelea hivi sasa, kwa mujibu wa vyanzo vya ndani, ni kuangalia nani
kati ya viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo atashika nafasi gani,
ingawa tayari maafikiano yanakaribia kufikia tamati.
Taarifa
zinasema kwamba, ikiwa Lowassa atagombea urais kupitia Ukawa akitokea
Chadema, basi mgombea mwenza – ambaye ndiye atakayekuwa Makamu wa Rais –
atakuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), mchumi Profesa Nguyulu
Ibrahim Haruna Lipumba.
Habari za
ndani zinaeleza kwamba chini ya makubaliano ya Ukawa ikiwa mgombea urais
atatoka Chadema, mgombea mwenza akitoka chama kingine itabidi ahame
chama chake ili aingie chama alicho mgombea urais ili kukidhi matakwa ya
kikatiba.
“Tutakaposhinda
uchaguzi, kama makamu wa rais atatoka CUF itabidi kila akitoka katika
ofisi ya makamu wa rais, kituo cha kwanza atasimama Makao Makuu ya CUF
kwa ajili ya kupeleka taarifa na kupata baraka za chama katika masuala
muhimu,” chanzo kimoja kilinukuliwa kikisema.
“Kazi
imekwisha, hivi sasa watu wanapanga mikakati ya nani awe nani baada ya
uchaguzi, najua Lipumba atakuwa makamu wa rais na hiyo inaweza
kuimarisha serikali kwa sababu Lowassa ni mchapakazi asiyependa
masikhara na makamu wake ni mchumi aliyebobea,” alisema mmoja wa watu
walio karibu na viongozi hao.
Hata
hivyo, katika upangaji wa uongozi, inabainishwa kwamba Dk. Wilbrod Peter
Slaa ndiye aliyepangwa kuwa Waziri Mkuu na kujenga safu imara ya
uongozi wa juu wa taifa, lakini kitendo chake cha kukaa pembeni hivi
sasa kimeweka doa kambi hiyo ya Ukawa.
Vyanzo
hivyo vinawataja wabunge kadhaa wa vyama hivyo waliomaliza muda wao
kwamba ndio wanaopigiwa chapuo kuongoza wizara mbalimbali, japokuwa wapo
baadhi yao ambao wameanguka katika kura za maoni.
“Mhandisi
Mohammed Habib Juma Mnyaa ameshindwa kwenye jimbo lake la Mkoani huko
Pemba, lakini huyu jamaa ndiye anayefaa kuongoza Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia ambayo aliiongoza akiwa waziri kivuli.
“Yupo pia
Mhandisi aliyebobea, Dk. Emmanuel John Makaidi, ambaye anastahili
kuongoza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ufanisi mkubwa,” mjumbe mmoja
kutoka CUF.
Taarifa
hizo zinasema, Dk. Makaidi, Mwenyekiti wa chama cha NLD kinachounda
Ukawa ambaye alipata kuwa mwenyekiti wa klabu ya soka ya Simba kabla ya
kurithiwa na Juma Salum, anaweza kuteuliwa na rais kutoka kwenye ‘kapu’
badala ya kuingia majimboni kupigana vikumbo, fursa ambayo pia anaweza
kuipata Mhandisi Mnyaa.
Mwaka 2005 alishika nafasi ya saba kati ya wagombea urais 10 waliojitokeza na kupata kura 21,574 sawa na asilimia 0.19, akiwa nyuma ya Mchungaji Christopher Mtikila wa DP.
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe, anatajwa kwamba ataongoza Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wakati Mchungaji Peter Simon Msigwa
ataongoza Wizara ya Maliasili na Utalii.
Waziri wa
zamani wa Maliasili, Utalii na Mazingira, Juma Hamad Omar, ambaye
amepitishwa na CUF kugombea katika Jimbo la Wawi kuziba nafasi ya Hamad
Rashid Mohammed bado hajafikiriwa nafasi gani atapatiwa kutokana na
uzoefu wake, ingawa anatajwa kwamba anafaa kuongoza Wizara ya Mazingira,
lakini kashfa ya mkataba ‘haramu’ wa Loliondo inaweza kumtia doa.
Kumbukumbu
zinaonyesha kwamba, Juma Hamad Omar, ambaye aliongoza wizara hiyo
wakati wa serikali ya awamu ya pili, hatasahaulika kirahisi katika
historia ya uongozi wa wizara hiyo, kwani wakati wa uongozi wake ndipo
ilipotokea kashfa ya uuzwaji wa Pori la Loliondo kwa Mwana wa Mfalme wa
Falme za Kiarabu.
Kashfa
hiyo ni kati ya matukio makubwa yaliyotikisa nchi kwani ilisababisha
kuundwa kwa Kamati ya Bunge iliyoongozwa na Mateo Qaresi na chanzo cha
kuondolewa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wakati huo, Muhidin
Ahmad Ndolanga, ambaye alimchapa kibao Qaresi bungeni pale Karimjee.
Omar aliondoka katika wizara hiyo mwaka 1995 baada ya Rais Mkapa kuingia
madarakani.
Ifuatayo
ni orodha pendekezwa ya baadhi ya wizara za sasa (japokuwa kuna
uwezekano wa kuzipunguza ikiwa Ukawa wataingia madarakani ili kupunguza
matumizi ya serikali):
Waziri
katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora): Wilfred Muganyizi Lwakatare,
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, ambaye kwa sasa ameshinda
kura za maoni kugombea tena katika Jimbo la Bukoba Mjini.
Waziri
Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma): Profesa Kulikoyela
Kanalwanda Kahigi (Chadema), ambaye anagombea tena katika Jimbo la
Bukombe.
Waziri katika Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu): Joseph Roman Selesini (Chadema) anatetea nafasi yake katika Jimbo la Rombo.
Waziri
katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge): Rajab Mohammed
Mbarouk (CUF) ambaye alikuwa waziri kivuli katika Bunge lililopita na
anatetea nafasi yake katika Jimbo la Ole.
Waziri
katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi): David Ernest Silinde (Chadema),
ambaye licha ya kuwa waziri kivuli katika Bunge lililopita, alionyesha
umakini mkubwa hata wakati wa uwasilishaji wa bajeti kivuli. Anagombea
katika Jimbo la Momba mkoani Songwe.
Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira): Juma Hamad Omar (CUF) anagombea katika Jimbo la Wawi.
Waziri
katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano): Masoud Abdallah Salim (CUF)
ambaye anatetea tena nafasi yake katika Jimbo la Mtambile.
Waziri
katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji): Pauline Philipo
Gekul (Chadema) ndiye aliyekuwa waziri kivuli. Uwezo wake wa kujenga
hoja na kuzitetea ndio umemfanya hata akashinda kura za maoni katika
Jimbo la Babati Mjini mkoani Manyara.
Waziri wa
Fedha, Uchumi na Mipango: John Mnyika (Chadema), ambaye safari hii
anagombea katika Jimbo jipya la Kibamba badala ya Ubungo.
Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi: James Mbatia (NCCR-Mageuzi), ambaye
anagombea tena katika Jimbo la Vunjo, lakini atakumbukwa na wengi jinsi
alivyoipeleka mchaka mchaka serikali Bungeni kuhusu suala la mitaala ya
elimu.
Waziri wa
Maliasili na Utalii: Mchungaji Peter Msigwa (Chadema). Anafahamika vyema
jinsi alivyokuwa akipambana kufichua uovu katika wizara hiyo na hoja
zake ndizo zilichangia wakurugenzi takriban saba wa wizara hiyo
kutimuliwa.
Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi: Halima James Mdee (Chadema). Ni
mmoja kati ya wabunge imara ambaye tangu ameingia mwaka 2005, kwanza
kupitia Viti Maalum na baadaye jimboni Kawe, aliweza kufichua uozo wa
serikali katika uuzaji wa ardhi na kusababisha migogoro mingi.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto: Magdalena Sakaya (CUF).
Wizara ya
Katiba na Sheria: Tundu Antipas Lisu (Chadema), ndiye Mwanasheria Mkuu
wa Chadema na alikuwa Mnadhimu Mkuu (Chief Whip) wa upinzani.
Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko: Dk. Emmanuel John Makaidi (NLD).
Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu: Mhandisi Mohammed Habib Juma Mnyaa (CUF).
Wizara ya Kazi na Ajira: David Kafulila (NCCR-Mageuzi).
No comments:
Post a Comment