Mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli amesema serikali yake itaimarisha masilahi ya wafanyakazi wote wakiwamo polisi, ili wasiwe wanalinda na kukosa fedha za kula nyumbani na hatimaye kusinzia vituoni na kunyang’anywa silaha.
Hii
ni mara ya kwanza kwa Dk Magufuli kuzungumza kwa kina mpango wake wa
kudhibiti wimbi la uvamizi wa vituo vya polisi, linalozidi kukua nchini
na kuhatarisha maisha ya polisi na wananchi.
Akiwahutubia
wakazi wa Makete, Dk Magufuli alisema anataka polisi wawe wanakwenda
kazini wameshiba, hata jambazi akivamia wanamwua hapohapo bila kusubiri
polisi jamii.
“Nazungumza
kwa ukweli kwa sababu jeshi letu linatakiwa liheshimike, siyo mnakaa
kwenye kituo watu wanachukua silaha wakati na ninyi mna silaha, “
alisema na kushangiliwa.
“Ninataka
jeshi ambalo likimuona jambazi linamwasha kwa sababu yeye alikuja
kuwawasha. Nataka iwe jiwe kwa jiwe, moto kwa moto, mguu kwa mguu,
kichwa kwa kichwa, sikio kwa sikio, hayo ndiyo tunayoyataka.”
Dk
Magufuli alisema maneno hayo huenda yakaonekana makali kwa baadhi ya
watu lakini “hilo ndilo jibu”, na kwamba suala hilo linatakiwa kufanywa
kwa kuzingatia sheria na utu wa binadamu.
Kauli
hiyo aliirudia tena Njombe Mjini akisisitiza wakati wake “jambazi akija
mchape risasi,” ili nchi iwe na amani na kuwafanya wananchi wafanye
biashara zao kwa usalama kama nchi nyingine zilizoendelea.
Barabara
Dk
Magufuli aliahidi kujenga barabara ya lami kuanzia Njombe kupitia
Makete hadi Mbeya, na kueleza kuwa usanifu na upembuzi yakinifu
vimeshafanyika na kilichobaki ni kuanza ujenzi akiingia madarakani.
Pia,
aliahidi kuboresha maisha ya wasanii nchini, akiahidi kuwaanzishia
mfuko maalumu hivyo kuwataka wasihofu kuwa anawatumia tu kwa sasa wakati
wa kampeni, bali atawajali hata baada ya kushinda.
Mgombea
huyo aliyeingia mkoa wa tano wa kampeni zake alizungumzia ilani ya CCM,
hasa suala la elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne,
mikopo ya Sh50 milioni kwa kina mama na vijana kila kata, kuboresha
huduma za umeme, afya, maji, pembejeo na kuimarisha masoko kwa wakulima.
Waziri
huyo wa Ujenzi, jana alikutana na Naibu wake, Gerson Lwenge katika
mkutano uliofanyika Makoga, Njombe Magharibi na kila mmoja kumnadi
mwenzake.
Lwenge alisema Dk Magufuli kuwa amefanya naye kazi na kwamba ni mfanyakazi na “mkali kwelikweli anayetenda haki.”
Azungumzia afya yake
Akizungumzia
afya yake, aliwataka Watanzania kutohofia akisema yupo imara.
Aliwaambia wakazi wa Makoga wilayani Wanging’ombe kuwa yuko timamu na
atapambana hadi mwisho.
Alieleza
kuwa kuna uzushi umezuka kwenye mitandao ya kijamii kuwa anaumwa na
amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), jambo ambalo siyo
kweli.
No comments:
Post a Comment