CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM), kinatarajiwa kuzindua kampeni zake za urais,
ubunge na udiwani nchi nzima katika viwanja vya Jangwani leo, katika
mkutano utakaorushwa moja kwa moja na televishe
Katika
uzinduzi huo, CCM pia inatarajiwa kuweka ilani yake ya uchaguzi
hadharani, itakayonadiwa na mgombea urais wake, Dk John Magufuli na
wagombea wengine wa ubunge na udiwani nchi nzima.
Moja
ya mambo ambayo CCM inatarajiwa kufafanua ni matumaini makubwa ya uwezo
wa mgombea wake katika kusimamia utekelezaji wa ilani hiyo, kutokana na
historia yake ya utendaji ndani ya Serikali katika nafasi mbalimbali
alizokabidhiwa, ikiwemo Waziri wa Ujenzi.
Wageni mbalimbali pia wamealikwa kuhudhuria uzinduzi huo vikiwemo pia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa CCM Mkoa, Juma Simba alisema vile
vile wanatarajia wageni kutoka ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam
kuhudhuria mkutano huo leo.
“Tumetuma
mialiko ya mkutano wa kesho (leo) sio tu kwa wana CCM wenzetu bali pia
kwa vyama vingine vya siasa ikiwa ni pamoja na kwa vyama vya ‘Ukawa’,” alisema.
Simba
alisema mkutano huo utakuwa mkubwa na wa aina yake ambapo viongozi
mbalimbali wa chama wanatarajiwa kushiriki na kwamba mkutano huo ratiba
yake itaanza asubuhi saa tatu kwa burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali
na wananchi kuendelea kuwasili uwanjani.
Sifa
za Magufuli Mgombea huyo amekuwa akitajwa kuwa na sifa ya mchapakazi,
makini, asiyependa uvivu, ambapo Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete
alimpachika jina “Tingatinga”.
Rais
Kikwete alimpachika Magufuli jina hilo, baada ya kutangazwa kuwashinda
makada wengine wawili waliokuwa wakiwania kuteuliwa kuwania urais
kupitia chama hicho katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika
Dodoma.
“Kila
mtu anaitwa jembe lakini huyu ni zaidi ya jembe. Ni tingatinga…
Magufuli ni bulldozer. Magufuli havumilii ujinga, ni mtu ambaye anataka
kuona kazi zake zinafanyika kama alivyoagiza,” alikaririwa akisema.
Kikwete
aliendelea kummwagia sifa Dk Magufuli kuhusu utendaji wake akisema kuwa
alipokuwa akifuatilia makandarasi kwenye miradi ya ujenzi, alidiriki
kuwatimua pale alipobaini walikuwa wakifanya kazi kinyume na
makubaliano.
Baadhi
ya watu waliofanya naye kazi wamekaririwa wakisema iwapo atachaguliwa
kuwa rais basi wavivu wajitayarishe kukimbia kwani Waziri huyo ni mchapa
kazi wa hali ya juu.
No comments:
Post a Comment