Taarifa
kutoka ndani ya TRA zinapasha kuwa tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
awasimamishe kazi maofisa kadhaa wa mamlaka hiyo, Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na kitengo cha uchunguzi cha mamlaka hiyo, hivi sasa wapo
kwenye msako wa kubaini ukwasi wa wafanyakazi wake.
Kwa
mujibu wa gazeti la Mtanzania, juzi maofisa wa kitengo cha uchunguzi
kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, walifika katika eneo la Tegeta
Salasala wilayani Kinondoni na kuvamia nyumba mbili za wafanyakazi wa
mamlaka hiyo.
Katika nyumba hizo, wafanyakazi hao kila mmoja alikutwa na kiasi kikubwa cha fedha ndani kuliko kiwango cha mshahara anaolipwa.
“Walivamiwa
wafanyakazi wawili (majina yanahifadhiwa), ambapo katika kila nyumba
zilikutwa fedha nyingi. Kwa mtu wa kwanza zilikutwa Sh milioni 200 na
yule wa jirani yake pia alikuwa na zaidi ya shilingi milioni 150.
“Tangu
kuanza kwa msako huu wafanyakazi wengi wamekuwa hawana amani kabisa, na
hata wengine wanasema wazi kama wangekuwa na uwekezaji wa nje ya nchi
wangeondoka kabisa nchini,” kilisema chanzo cha gazeti hilo.
Kutokana
na hali hiyo, baadhi ya wafanyakazi hivi sasa wamelazimika kuzikimbia
nyumba zao na kuishia kulala hotelini huku wakienda kazini wakiwa na
hofu.
Hivi
karibuni, vyombo vya habari viliripoti kuwa Kamishna wa Forodha wa TRA,
Tiagi Masamaki, aliyesimamishwa kazi pamoja na vigogo wengine wa
mamlaka hiyo kutokana na upotevu wa kontena 349 zenye thamani ya Sh
bilioni 80, amebainika kumiliki nyumba 73.
No comments:
Post a Comment