Mkutano Mkuu wa Chadema, kwa kauli moja, jana umempitisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Akihutubia mkutano huo mkuu wa Chadema kwa mara ya kwanza, Lowassa alisema chama hicho kupitia Ukawa kitachukua nchi mapema asubuhi Oktoba 25.
Alisema Watanzania wanajua kuwa Chadema wamepania, wamejipanga na wana uhakika wa kukamata dola mwaka huu.
“Nilianza
na safari ya matumaini, lakini sasa nasema hii ni Safari ya Mabadiliko
nje ya CCM, tutakamata nchi mapema kabisa asubuhi,” alisema Lowassa.
Hata
hivyo, Lowassa alitahadharisha kuwa kuing’oa CCM ni kazi kubwa kama
hakutakuwa na mipango na malengo huku akisema hakujiunga na chama hicho
akiwaza kushindwa na kwamba hana msamiati wa kushindwa na wala hakwenda
kwa bahati mbaya, bali alijiridhisha na kukubaliana na familia yake hadi
kufikia uamuzi huo.
“Nimekuja
Chadema nikijua kuwa kazi ya chama ni kushika dola na kama si hivyo,
hakuna sababu ya kuwa chama, nimejiandaa vizuri kushika dola… watu
wanasema Chadema haiwezi, Tanu ilipewa nchi ikiwa na miaka saba, sasa
ninyi mna miaka 23,” alisema na kushangiliwa.
Aliongeza,“Najua
kazi ni kubwa na mnajitolea, ndiyo maana chama kina nguvu na moyo kama
CCM ya zamani si ya sasa, ndiyo maana tumeikimbia,” alisema Lowassa.
Alisema atapita kila jimbo kutengeneza mipango ya ushindi kwa kufanya kampeni za kistaarabu huku akionya... “Mradi wasiibe kura zetu.”
Mgombea mwenza, Duni Haji aliirushia kijembe CCM kuwa inafanya wananchi wawe maskini ili iendelee kuwatawala.
Akizungumza
baada ya kuteuliwa na chama hicho kuwa mgombea mwenza, Duni alisema,
CCM haiwezi kuwasaidia wananchi kutoka kwenye umaskini kwa sababu sera
yao ni umaskini.
“Miaka
ya 70 hatukuwa na neno changudoa, jambazi wala panya road. Haya
yamekuja kutokana na kushindwa kwa utawala wa CCM. Ukawa tumedhamiria
kuchukua madaraka ya nchi hii ili kuleta mabadiliko,” alisema.
Alisema
wananchi wamejenga imani na matumaini kwa makubaliano yaliyofanyika
jangwani, walipotia saini hati ya makubaliano inayoruhusu vyama
kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja kwenye kila nafasi ya uongozi
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Akimzungumzia mgombea urais, Duni alisema: “Siyo
jambo rahisi kufanya uamuzi mgumu kama aliofanya Lowassa. Wengi bado
wapo CCM licha ya kuwa hawapendi mfumo wa chama chao, alichokifanya
Lowassa ni ujasiri mkubwa.”
Hata
kwake, alisema halikuwa jambo rahisi kuihama CUF na kujiunga na
Chadema. Alisema kuwa alikubaliana na viongozi wake, Profesa Lipumba na
Maalim Seif Sharif Hamad aende Chadema ili Ukawa ilete ukombozi katika
Taifa.
“Profesa
Lipumba ananipenda sana na ananikubali haswa… na anajua kuwa hiki ni
kifaa. Lakini alikubali nijivue uanachama wa CUF ili niende Chadema
kuongeza nguvu ya kuleta mabadiliko, nina imani Ukawa tutashika dola
ifikapo Oktoba 25,” alisema.
Alisisitiza
kuwa Ukawa ndiyo ufumbuzi wa matatizo ya Watanzania akisema umoja huo
unaungwa mkono na wananchi wengi, hivyo hana shaka kwamba utashinda
katika uchaguzi ujao.
“Nilikuwa
mwanachama wa ASP nilipokuwa kidato cha pili. Nilipoona mambo
yanabadilika nami nilibadilika. Lengo kuu la kupigania uhuru lilikuwa ni
Mwafrika kumtawala Mwafrika mwenzake ili amlinde, lakini lengo hilo
sasa limepotea.
“Ninashangaa
kuona askari wa kimaskini aliyepewa bunduki kuwalinda wananchi,
anageuka na kuwapiga risasi maskini wenzake, huu ni udhalimu
uliotengenezwa na Chama cha Mapinduzi,” alisema.
No comments:
Post a Comment